SIMULIZI FUPI : GRACE WA MWANZA - Linda Penzi Lako

Breaking

Pages

Jumamosi, 25 Agosti 2018

SIMULIZI FUPI : GRACE WA MWANZA


Sura yake iliyokuwa imepauka, nywele zake ndefu zilizokosa matunzo na midomo iliyokauka sana haikuweza kuificha historia ya sura yake jinsi ilivyokuwa ikivutia miaka minne nyuma.
  
Alikuwa amejikunyata mitaa ya Kariakoo, mbele yake pakiwa na sufuria dogo. Ndani yake pakiwa na matawi ya mchicha, yakiwa yamejinyaukia katika namna ya kutia kinyaa. Bila shaka hata yeye hakupendezwa kuyatazama majani yale.
Haikuwa mara ya kwanza kumuona binti Yule akiwa eneo lilelile na katika hali ileile ya majonzi.
Ama kwa hakika alikuwa anasikitisha!


Sijui ni kitu gani kiliniaminisha kuwa anaweza kuzungumza nami walau kwa dakika tano. Kwa sababu niliamini kuwa hanitambui tena!!
Nikamkaribia na kuulizia bei ya matawi yale ya mchicha.
Alibabaika katika kunijibu na kisha akanitajia bei ambayo niliamini hata yeye alitamka ilimradi aipate ile pesa.
Nikatoa kiasi cha pesa aliyoihitaji lakini sikuishia kumpatia tu. Badala yake nilimvuta kando na kisha nikauvunja ukimya. Nikamweleza kuwa haikuwa mara ya kwanza kuonana naye, na kidogo ningependa kuzungumza naye.
Akanitazama kabla ya kutoa tabasamu hafifu sana. Sikuendelea kumtazama machoni badala yake niliinama na hapo nikaiona miguu yake ilivyopauka na pia akiwa amevalia kandambili zenye rangi tofauti.
“Ni kipi unahitaji kujua kutoka kwangu ewe mwanaume!” aliniuliza huku akipepesa macho huku na kule.
Kabla sijasema lolote akajitambulisha kwa jina lake.
“Naitwa Grace wa mwanza… sijui iwapo unalo jingine” akataka kuondoka nikamdaka mkono, huku nikimkumbushga kuwa bado sijampatia pesa yake.


Akanyoosha mkono ili nimpatie pesa lakini badala ya kumpa pesa nikamwita kwa jina ambalo kamwe hakulitegemea.
“Mwamvita! Nini kilikusibu” nikamuuliza.
Macho yalimtoka, akanitazama mara mbilimbili asipate kunikumbuka. Nilipoligundua hilo nikajitambulisha jina langu.
Akanisogelea na kisha kunikumbatia kwa nguvu sana, na hapo nikahisi majimaji ya joto yakipenya katika mwili wangu.
Bila shaka alikuwa analia!
Sikutaka umati utushangae, nikamsogeza Yule binti kando, tukaufikia mgahawa Fulani usiokuwa na watu wengi. Akaketi mkabala na kiti nilichokuwa nimekaa mimi.


Hata kabla sijaanza kuzungumza lolote. Huku akiwa anatokwa machozi Grace wa Mwanza akaanza kunielezea jambo ambalo lilimfanya awe vile ninavyomuona wakati huu.
“Jimmy, naujutia usichana. Usichana ambao kamwe hautarejea kamwe, najutia kiburi changu na huu ule urembo ulionizuzua. Najutia hata marafiki niliowachagua, walikuwa marafiki wabaya sana. Walinitafutia wanaume na nilitumika mimi lakini pesa tulitumia pamoja nao. Ama!! Nilikuwa bwege
Wakanieleza kuwa mimi ni mrembo na sina hadhi ya kuishi mjini Mwanza, maneno yao yale ya kipuuzi yakaniingia kichwani. Hatimaye wakaniunganisha na mwanaume ambaye aliniahidi kuwa ananileta jijini Dar es salaam kwa madhumuni mawili. Kunitafutia kazi na kisha kunioa kabisa niwe mkewe wa ndoa.


Jimmy, mama yangu alinikanya huku analia. Alinisihi sana nisiondoke Mwanza. Nikamuigizia kuwa nimemuelewa akapata amani ya moyo, lakini haikuwa vile. Nikaondoka Mwanza huku nikijisemea kuwa kama yeye mama aliolewa na baba yangu basi name ni haki yangu kuolewa.
Jimmy, haikuwa ndoa wala haikuwa kazi. Ama kwa hakika Dar es salaam sio tu ni mkoa wa kipekee bali ni nchi ndani ya nchi ya Tanzania.
Nchi hii inaweza kukufanya uwe mwehu ghafla na usipate hata mtu mmoja wa kukushangaa.
Jimmy! Yule kaka aliyejifanya mume mtarajiwa alinitelekeza kama utani vile baada ya kumgomea aliniponitaka nijiunge katika danguro na kuuza mwili wangu.


Kutelekezwa huko ukawa mwanzo wa kujiuza bila hiari, nimetumika Jimmy. Nimetumika sana. Hii ni laana Jimmy. Laana kutoka kwa mama ambaye nilisikia kuwa aliugua sana na sikurejea kumuuguza mama yangu.
Nimeteseka hadi hatua hii unionayo, sina thamani hata ya kukaa ndani ya hoteli hii. Mimi ni mchafu, na sijui kama sijaathirika. Nahisi mimi si mzima.
Hilo halinishtui lakini Jimmy huenda ni Mungu amekuleta ukutane nami leo, nakusihi Jimmy. Nichukue Jimmy, najua haiwezi kuwa kimapenzi kama ulivyohitaji wakati ule lakini nichukue kama mwanadamu tu anayejutia kila jambo alilolifanya.


Nichukue unirejeshe nyumbani…. Nimeteseka Jimmy imetosha!!
Nirejeshe Mwanza Jimmy, nikateseke na kufia huko. Naomba usiniache Jimmy. Wananibaka kila siku…. Wananitukana kila kukicha… sina amani hata chembe… sitaki kufia katika nchi hii iliyo ndani ya nchi. Nchi isiyotambua nini maana ya utu, nchi inayothamini pesa kuliko kitu chochote, nchi ambayo ukabila hakuna lakini undugu pia haujulikani.
Nitoe katika nchi hii Jimmy.. nirejeshe nyumbani”

Alishindwa kuendelea kuzungumza Grace wa Mwanza. Akanifuata nilipokuwa, akapiga magoti na kuendelea kusihi. Nilijikaza nisitokwe na tone la chozi lakini haikuwezekana, nikatokwa machozi. Nikamyanyua na kuabiri bajaji ikatupeleka hoteli niliyokuwa nimefikia.
Nikapanga safari ya upesi upesi.
Siku iliyofuata tukaondoka na Grace wa Mwanza… njia nzima alikuwa amechangamka sana. Alikuwa anazungumza sana huku mara kwa mara akijiuliza ni kwa namna gani ataulilia msamaha kutoka kwa mama yake.
Baadaye alisinzia! Na huo nd’o wakati ambao niliutumia kutafakari. Niliumia sana kwa sababu Grace hakuwa anaujua ukweli.


Hakujua kuwa yule mama aliyesikia kuwa aliugua basi aliaga dunia kwa ugonjwa uleule.
Nilihofia kumweleza maana ningeikatili furaha yake. Na huenda lingeweza kuzuka tatizo jingine.

Tulifika Mwanza usiku sana, nikachukua vyumba viwili. Tukapumzika na asubuhi nikamwongoza Grace hadi pale palipoitwa nyumbani kwao.
Hapakuwa na nyumba bali gofu. Mimi sikuwa jasiri wa kumueleza nini kilichotokea. Bali majirani tuliowakuta pale ndio waliomuweka chini na kuzungumza naye.

Naam! Siku nne baadaye mwili wake ulikutwa ukiwa unaning’inia porini. Watu waliofika wa kwanza eno la tukio walibahatika kuuona ujumbe uliouacha.
“Sina mama, sina baba, sina rafiki wa dhati bali nina rafiki mmoja tu mbaya…nina UKIMWI… Siwezi kuishi na rafiki huyu mbaya.
Wanizike watu wema!!


JIFUNZE: Wazazi ni nguzo muhimu. Tafadhali wasikilize, waelewe wasemacho. Wana kitu cha ziada ambacho, hata ufanye vipi hauwezi kuwa nacho.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni